[ PDF Version ]
Ombi la Mjumbe wa Bwana
Aprili 1, 1903 (Muswada 16, 1903)
Ombi hili la Ellen G White liliombwa wakati wa mkutano wa asubuhi uliofanyika wakati wa Session ya General Conference ya mwaka wa 1903, kule Oakland, California, Marekani. Mambo makuu katika mkutano huu yalikuwa yakihusu kurekebishwa kwa kujipanga upya jinsi ya kuongoza General Conference ya mwaka wa 1901, umiliki wa kanisa wa Sanitarium ya Battle Creek, na makao makuu ya Nyumba ya uchapaji ya Review na Herald.
Taasisi zote mbili zilikuwa zimeteketezwa kwa moto. Jengo la makao makuu la sanitarium liliteketea mnamo Febrari 18, 1902, na Jengo la kati la Uchapishaji lenyewe likiwa limeteketea Desemba 30, 1902
Baba wetu wa Mbinguni, wewe umesema ,”Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa“
[Mathayo 7:7].
Baba wetu wa Mbinguni tunahitaji Roho wako Mtakatifu. Hatutaki kufanya kazi hii peke yetu wenyewe tunahitaji kuwa na ushirikiano na Mungu. Tunahitaji kuwa mahali ambapo Roho Mtakatifu wa Mungu atakuwa juu yetu akitupatia uamsho na nguvu itakasayo. Mungu hebu leo asubuhi hii uweze kuonekana kati yetu! Tunakuomba ufagilie mbali ukungu na wingu la giza.
Tunakuja Kwako, wewe Mkombozi wetu; tunakuomba katika jina la Kristo, na kwa ajili yake- kwa ajili ya Mwanao, Baba yetu; kwamba utaonyesha Utukufu Wako kwa watu wako waliohudhuria hapa leo. Tunahitaji hekima, tunahitaji haki, tunahitaji ukweli, tunahitaji Roho Mtakatifu kuwa pamoja nasi.
Wewe Mungu wetu umetupatia kazi kubwa mbele zetu ambayo inahitaji kuendelezwa mbele kwa niaba ya wale ambao wako kwenye kweli na kwa niaba ya wale ambao bado hawajatambua Imani yetu; na Bwana wetu, tunakusihi kama ulivyo wapatia kila mtu kazi yake ya kutenda, tunakuomba na kukusihi uweze kutuonyesha katika akili zetu uzito wa kazi utakaopewa kila roho iliyoko hapa kufuatana na uteule wako. Tunahitaji kuhakikishwa ; tunahitaji kutakaswa kikamilifu kwa kindani. Tunahitaji kuwa watu tunaostahili kufanya kazi hii; hapa na hapa kwenye kungamano hili la General Conference; tunataka kuona ufunuo wa Roho ya Mungu. Tunataka nuru, Mungu wetu – Wewe ndiwe Nuru. Tunataka kweli, Bwana wetu – Wewe ndiwe Kweli. Tunataka njia sahihi – Wewe ndiwe Njia.
Bwana wetu, Ninakusihi kuwa sisi sote tuwe na hekima ya kuwa wazi na kufungua kila mmoja wetu mioyo yetu ili Yesu Kristo aingie ndani yetu, ili kupitia kwa njia ya Roho Mtakatifu aweze kutujenga na kututengeneza upya, katika mfano mtakatifu. Baba yangu, Baba yangu, yeyusha na kuitiisha mioyo yetu. Ni hitaji letu kuu asubuhi ya leo kujitoa kikamilifu kwako; tuna hitaji kusalimisha matakwa yetu, njia yetu, na hata maamuzi yetu ambayo yamekuwa kinyume na njia na mapenzi ya Mungu; tuna hitaji kukubali njia ya Bwana, mapenzi ya Bwana, na mwongozo wa Bwana. Njoo, Njoo ndani ya mioyo yetu asubuhi hii, na washa mioyo yetu, ya wakubwa na wadogo. Mungu wangu kwa njia ya pekee gusa mioyo ya wale ambao wana fanya kazi ya kuendesha kweli ya injili, ili kwamba wote waweze kuangazwa na miale ya neno lako, ili maagizo yako yaweze kuelewekwa na binadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu wa Mungu aishie juu.
Tunakubali kuwa hatujaheshimu jina Lako kama ipasavyo. Tunakubali asubuhi hii tunahitaji mioyo yetu ipondwe. Ni shauku letu tunahitaji kuongolewa tena; tunahitaji kutambua Yesu ninani kwetu, na sisi ninani na tunaweza kuwa wafanyakazi pamoja naye. “Maana sisi tuwafanya kazi na Mungu “
[1 Wakorintho 3:9]
Baba yangu, hebu kila roho ambayo imechanganyikiwa, kila roho ambayo haiwezi kuelewa and kuona njia, uonyeshe njia ambayo itatoa ukwasi na wingu ili Jua la utakatifu liangaze katika vyumba vya mawazo na katika hekalu la roho. Utuoshe Bwana, nasi tutakuwa safi. Utuyeyushie rehema, rehema zitokazo kwako, Njoo katika kila moyo; na hapo tutakapokuwa tumetambua rehema na wema wako na upendo wa Mwokozi, mioyo yetu itakuwa imeungana tena, tutafanya kazi kwa mpigo mmoja na sote tutasimama bega kwa bega katika kusukuma kazi yako.
Hatuwezi kuthubutu kuwa tofauti, Mungu wetu, hatuwezi kufanya kazi tukipingana kati yetu. Ni lazima tu kuamini. Tunakuomba asubuhi ya leo utatuma Roho wako Mtakatifu ili aweze kutushukia ndani yetu. Tuko tayari kumpokea Mfariji wetu, tunafungua mioyo yetu, na kumkaribisha Mwokozi ndani. Tunakupenda Mungu wetu. Tunaona upendo usio na tufani ndani yako na niombi letu kuwa kila roho itakuangalia wewe. Wewe ni Mwanzilishi na Mtimizaji wa Imani yetu.
Njoo, Bwana Yesu, njoo na utuchukue kama tulivyo, na utuvalishe vazi lako takatifu. Toa dhambi zetu, Mwokozi Wetu. Ulikuja hapa duniani kufanya hicho. Tunaungama makosa yetu; tunasikitika kwa kile kilichotufanya tukatoka kwako, na tunaomba utusamehe tulipokukosea, ili tuweze kuonyesha ulimwengu kuwa tuna Mwokozi ambaye yuko tayari kutuondolea dhambi zetu na kutupatia vazi lake la Haki
Bwana, tunakukubali sasa. Tunakupokea sasa. Tunakuamini sasa; na tunakuomba ulete Roho Mtakatifu wako akae juu yetu saa hii. Saa hii tunaomba utembee ndani ya nyumba yetu hii; Tunaomba Bwana wetu Malaika wanaoambatana nawe watembelee kila kiti na kila moyo; Na nakuomba kila mtu ajitambue kama “Mimi” ningelifanya kitu gani. Naomba Mungu wangu kila mtu asimwangalie mtu, bali amwone Yesu Kristo – Yeye ambaye ametufia kutuokoa. Tumeokolewa na Wewe, Bwana, tunakutazama Wewe, Bwana. Nguvu yako na itushukie juu yetu, itwambie kuwa dhambi zetu zime samehewa, Wewe umeahidi kuwa, “Nita kupatia moyo mpya.”
[Ezekieli 36:26]
Tunahitaji mioyo yetu iwe mipya, Bwana tunatamani iwe hivo.
Bariki ndugu zetu wanaohudumu. Bariki wale wote wanaofanya kazi kwenye ofisi za taasisi zetu. Hatutaki ukaziharibu taasisi hizi; hatutaki kuona mvuto wao ikifutiliwa mbali. Tunaomba utoe kile ambacho si kizuri katika moyo, maisha, na tabia ya kila mfanya kazi, ili uweze kutumia kila taasisi uliyo iweka Wewe mwenyewe kutukuza jina lako. Tunahitaji kila taasisi iliyoko kati yetu.
O Mwokozi wangu, Wewe ambaye umeonyesha huruma kwetu sote, tunakuomba tena, utupatie sehemu kubwa ya rehema Yako, wingi Wako, huruma Yako, upendo Wako wa daima, Njoo, Bwana Yesu, na utufanye kuwa washiriki wa mambo ya kiroho Yako, ili tuweze kushinda ufisadi ambao uko ulimwenguni kwa njia ya tamaa. Roho ya Kristo, upendo wa Mungu, ufariji kila moyo asubuhi ya leo. Fukuza giza, epusha nguvu za udanganyifu za adui, na sauti Yako na Roho Yako na upendo Wako uje ndani ya roho zetu, ili tuweze kukaa pamoja na Yesu Kristo mahala pa kimbingu; na jina Lako litakuwa na utukufu wote. Amina
Imetafsiriwa na Dr Baraka G. Muganda